'Umaskini si kilema'
Umaskini kizungumkuti
Linifanya npigwe buti
Sababu sina suti
Nliitamani mauti
Tatizo sina mali
Ufukara yangu hali
Kazi yangu uhemali
Linihepa wanamwali
Nlimuomba Maulana
Usiku wote na mchana
Aniondolee mbaya dhana
Niufurahie ujana
Maombi yangu lijibiwa
Hivi leo meajiriwa
Walonicheka meduwaa
Mambo yangu sasa 'waa'
Allihamdullillah nashkuru
Kamwe tena skufuru
Natoa pia ushuru
Maisha yangu sasa huru
Mambo menibadilikia
Sili tena na surua
Nala chakula murua
Sifanyi tena vibarua
Mbona leo wanifuata
Si weye linikataa
Kaniona sitopata
Niache nilie ngwata
Umaskini si kilema
Nlitengwa kama ukoma
Wanadamu sio wema
Naungama nshakoma
Nkiaga nakujuza
Nakuona kama ajuza
Mengi mwenyewe utajaza.
Namshukuru alonizaa
Sina hofu ushajua
Nmelitunda langu ua
Tena zuri lochanua
Wivu wako takuua
Nakuacha nao wasia
Siwatenge wao wakia
Upatacho saidia
Allah atakujazia